KUSOMA KITABU CHA ZABURI  DAY 07

| Makala

 

Zaburi 31

1  Nimekukimbilia Wewe, Bwana, Nisiaibike milele. Kwa haki yako uniponye,

2  Unitegee sikio lako, uniokoe hima. Uwe kwangu mwamba wa nguvu, Nyumba yenye maboma ya kuniokoa.

3  Ndiwe genge langu na ngome yangu; Kwa ajili ya jina lako uniongoze, unichunge.

4  Utanitoa katika wavu walionitegea kwa siri, Maana Wewe ndiwe ngome yangu.

5  Mikononi mwako naiweka roho yangu; Umenikomboa, Ee Bwana, Mungu wa kweli.

6  Nawachukia wao washikao yasiyofaa yenye uongo; Bali mimi namtumaini Bwana.

7  Na nishangilie, nizifurahie fadhili zako, Kwa kuwa umeyaona mateso yangu. Umeijua nafsi yangu taabuni,

8  Wala hukunitia mikononi mwa adui; Miguu yangu umeisimamisha panapo nafasi.

9  Ee Bwana, unifadhili, maana ni katika dhiki, Jicho langu limenyauka kwa masumbufu, Naam, mwili wangu na nafsi yangu.

10  Maana maisha yangu yamekoma kwa huzuni, Na miaka yangu kwa kuugua. Nguvu zangu zinatetemeka kwa uovu wangu, Na mifupa yangu imekauka.

11  Kwa sababu ya watesi wangu nimekuwa laumu, Naam, hasa kwa jirani zangu; Na kitu cha kutisha kwa rafiki zangu; Walioniona njiani walinikimbia.

12  Nimesahauliwa kama mfu asiyekumbukwa; Nimekuwa kama chombo kilichovunjika.

13  Maana nimesikia masingizio ya wengi; Hofu ziko pande zote. Waliposhauriana juu yangu, Walifanya hila wauondoe uhai wangu.

14  Lakini mimi nakutumaini Wewe, Bwana, Nimesema, Wewe ndiwe Mungu wangu.

15  Nyakati zangu zimo mikononi mwako; Uniponye na adui zangu, nao wanaonifuatia.

16  Umwangaze mtumishi wako Kwa nuru ya uso wako; Uniokoe kwa ajili ya fadhili zako.

17  Ee Bwana, nisiaibishwe, maana nimekuita; Waaibishwe wasio haki, wanyamaze kuzimuni.

18  Midomo ya uongo iwe na ububu, Imneneayo mwenye haki maneno ya kiburi, Kwa majivuno na dharau.

19  Jinsi zilivyo nyingi fadhili zako Ulizowawekea wakuchao; Ulizowatendea wakukimbiliao Mbele ya wanadamu!

20  Utawasitiri na fitina za watu Katika sitara ya kuwapo kwako; Utawaficha katika hema Na mashindano ya ndimi.

21  Bwana ahimidiwe; kwa maana amenitendea Fadhili za ajabu katika mji wenye boma.

22  Nami nalisema kwa haraka yangu, Nimekatiliwa mbali na macho yako; Lakini ulisikia sauti ya dua yangu Wakati nilipokulilia.

23  Mpendeni Bwana, Ninyi nyote mlio watauwa wake. Bwana huwahifadhi waaminifu, Humlipa atendaye kiburi malipo tele.

24  Iweni hodari, mpige moyo konde, Ninyi nyote mnaomngoja Bwana.


 


 

Zaburi 32

1  Heri aliyesamehewa dhambi, Na kusitiriwa makosa yake.

2  Heri Bwana asiyemhesabia upotovu, Ambaye rohoni mwake hamna hila.

3  Niliponyamaza mifupa yangu ilichakaa Kwa kuugua kwangu mchana kutwa.

4  Kwa maana mchana na usiku Mkono wako ulinilemea. Jasho langu likakauka hata nikawa Kama nchi kavu wakati wa kaskazi.

5  Nalikujulisha dhambi yangu, Wala sikuuficha upotovu wangu. Nalisema, Nitayakiri maasi yangu kwa Bwana, Nawe ukanisamehe upotovu wa dhambi yangu.

6  Kwa hiyo kila mtu mtauwa Akuombe wakati unapopatikana. Hakika maji makuu yafurikapo, Hayatamfikia yeye.

7  Ndiwe sitara yangu, utanihifadhi na mateso, Utanizungusha nyimbo za wokovu.

8  Nitakufundisha na kukuonyesha njia utakayoiendea; Nitakushauri, jicho langu likikutazama.

9  Msiwe kama farasi wala nyumbu, Walio hawana akili. Kwa matandiko ya lijamu na hatamu Sharti kuwazuia hao, au hawatakukaribia.

10  Naye mtu mwovu ana mapigo mengi, Bali amtumainiye Bwana fadhili zitamzunguka.

11  Mfurahieni Bwana; Shangilieni, enyi wenye haki Pigeni vigelegele vya furaha; Ninyi nyote mlio wanyofu wa moyo.


 


 

Zaburi 33

1  Mpigieni Bwana vigelegele, enyi wenye haki, Kusifu kunawapasa wanyofu wa moyo.

2  Mshukuruni Bwana kwa kinubi, Kwa kinanda cha nyuzi kumi mwimbieni sifa.

3  Mwimbieni wimbo mpya, Pigeni kwa ustadi kwa sauti ya shangwe.

4  Kwa kuwa neno la Bwana lina adili, Na kazi yake yote huitenda kwa uaminifu.

5  Huzipenda haki na hukumu, Nchi imejaa fadhili za Bwana.

6  Kwa neno la Bwana mbingu zilifanyika, Na jeshi lake lote kwa pumzi ya kinywa chake.

7  Hukusanya maji ya bahari chungu chungu, Huviweka vilindi katika ghala.

8  Nchi yote na imwogope Bwana, Wote wakaao duniani na wamche.

9  Maana Yeye alisema, ikawa; Na Yeye aliamuru, ikasimama.

10  Bwana huyabatilisha mashauri ya mataifa, Huyatangua makusudi ya watu.

11  Shauri la Bwana lasimama milele, Makusudi ya moyo wake vizazi na vizazi.

12  Heri taifa ambalo Bwana ni Mungu wao, Watu aliowachagua kuwa urithi wake.

13  Toka mbinguni Bwana huchungulia, Huwatazama wanadamu wote pia.

14  Toka mahali pake aketipo Huwaangalia wote wakaao duniani.

15  yeye aiumbaye mioyo yao wote Huzifikiri kazi zao zote.

16  Hapana mfalme aokokaye kwa wingi wa uwezo, Wala shujaa haokoki kwa wingi wa nguvu.

17  Farasi hafai kitu kwa wokovu, Wala hamponyi mtu kwa wingi wa nguvu zake.

18  Tazama, jicho la Bwana li kwao wamchao, Wazingojeao fadhili zake.

19  Yeye huwaponya nafsi zao na mauti, Na kuwahuisha wakati wa njaa.

20  Nafsi zetu zinamngoja Bwana; Yeye ndiye msaada wetu na ngao yetu.

21  Maana mioyo yetu itamfurahia, Kwa kuwa tumelitumainia jina lake takatifu.

22  Ee Bwana, fadhili zako zikae nasi, Kama vile tulivyokungoja Wewe.


 


 

Zaburi 34

1  Nitamhimidi Bwana kila wakati, Sifa zake zi kinywani mwangu daima.

2  Katika Bwana nafsi yangu itajisifu, Wanyenyekevu wasikie wakafurahi.

3  Mtukuzeni Bwana pamoja nami, Na tuliadhimishe jina lake pamoja.

4  Nalimtafuta Bwana akanijibu, Akaniponya na hofu zangu zote.

5  Wakamwelekea macho wakatiwa nuru, Wala nyuso zao hazitaona haya.

6  Maskini huyu aliita, Bwana akasikia, Akamwokoa na taabu zake zote.

7  Malaika wa Bwana hufanya kituo, Akiwazungukia wamchao na kuwaokoa.

8  Onjeni mwone ya kuwa Bwana yu mwema; Heri mtu yule anayemtumaini.

9  Mcheni Bwana, enyi watakatifu wake, Yaani, wamchao hawahitaji kitu.

10  Wana-simba hutindikiwa, huona njaa; Bali wamtafutao Bwana hawatahitaji kitu cho chote kilicho chema.

11  Njoni, enyi wana, mnisikilize, Nami nitawafundisha kumcha Bwana.

12  Ni nani mtu yule apendezwaye na uzima, Apendaye siku nyingi apate kuona mema?

13  Uuzuie ulimi wako na mabaya, Na midomo yako na kusema hila.

14  Uache mabaya ukatende mema, Utafute amani ukaifuatie.

15  Macho ya Bwana huwaelekea wenye haki, Na masikio yake hukielekea kilio chao.

16  Uso wa Bwana ni juu ya watenda mabaya, Aliondoe kumbukumbu lao duniani.

17  Walilia, naye Bwana akasikia, Akawaponya na taabu zao zote.

18  Bwana yu karibu nao waliovunjika moyo, Na waliopondeka roho huwaokoa.

19  Mateso ya mwenye haki ni mengi, Lakini Bwana humponya nayo yote.

20  Huihifadhi mifupa yake yote, Haukuvunjika hata mmoja.

21  Uovu utamwua asiye haki, Nao wamchukiao mwenye haki watahukumiwa.

22  Bwana huzikomboa nafsi za watumishi wake, Wala hawatahukumiwa wote wamkimbiliao.


 


 

Zaburi 35

1  Ee Bwana, utete nao wanaoteta nami, Upigane nao wanaopigana nami.

2  Uishike ngao na kigao, Usimame unisaidie.

3  Uutoe na mkuki uwapinge wanaonifuatia, Uiambie nafsi yangu, Mimi ni wokovu wako.

4  Waaibishwe, wafedheheshwe, Wanaoitafuta nafsi yangu. Warudishwe nyuma, wafadhaishwe, Wanaonizulia mabaya.

5  Wawe kama makapi mbele ya upepo, Malaika wa Bwana akiwaangusha chini.

6  Njia yao na iwe giza na utelezi, Malaika wa Bwana akiwafuatia.

7  Maana bila sababu wamenifichia wavu, Bila sababu wameichimbia shimo nafsi yangu.

8  Uharibifu na umpate kwa ghafula, Na wavu aliouficha umnase yeye mwenyewe; Kwa uharibifu aanguke ndani yake.

9  Na nafsi yangu itamfurahia Bwana, Na kuushangilia wokovu wake.

10  Mifupa yangu yote itasema, Bwana, ni nani aliye kama Wewe? Umponyaye maskini na mtu aliye hodari kumshinda yeye, Naam, maskini na mhitaji na mtu amtekaye.

11  Mashahidi wa udhalimu wanasimama, Wananiuliza mambo nisiyoyajua.

12  Wananilipa mabaya badala ya mema, Hata nafsi yangu ikaingia ukiwa.

13  Bali mimi, walipougua wao, Nguo yangu ilikuwa gunia. Nalijitesa nafsi yangu kwa kufunga; Maombi yangu yakarejea kifuani mwangu.

14  Nalijifanya kama kwamba ni rafiki au ndugu yangu, Naliinama nikilia kama aliyefiwa na mamaye.

15  Lakini nikijikwaa hufurahi na kukusanyana, Walinikusanyikia watu ovyo nisiowajua, Wananipapura wala hawakomi.

16  Kama wenye mzaha wakikufuru karamuni Wananisagia meno.

17  Bwana, hata lini utatazama? Uiokoe nafsi yangu na maharabu yao, Na mpenzi wangu na wana-simba.

18  Nitakushukuru katika kusanyiko kubwa; Nitakusifu kati ya watu wengi.

19  Walio adui zangu bure wasinisimange, Wanaonichukia bila sababu wasining'ong'e.

20  Maana hawasemi maneno ya amani, Na juu ya watulivu wa nchi huwaza hila.

21  Nao wananifumbulia vinywa vyao, Husema, Ewe! Ewe! Jicho letu limeona.

22  Wewe, Bwana, umeona, usinyamaze; Ee Bwana, usiwe mbali nami.

23  Uamke, uwe macho ili kunipatia hukumu Kwa ajili ya madai yangu, Mungu wangu na Bwana wangu.

24  Unihukumu kwa haki yako, Ee Bwana, Mungu wangu, Wala wasinisimangize.

25  Wasiseme moyoni, Haya! Ndivyo tutakavyo; Wasiseme, Tumemmeza.

26  Waaibishwe, wafedheheshwe pamoja, Wanaoifurahia hali yangu mbaya. Wavikwe aibu na fedheha, Wanaojikuza juu yangu.

27  Washangilie na kufurahi, Wapendezwao na haki yangu. Naam, waseme daima, Atukuzwe Bwana, Apendezwaye na amani ya mtumishi wake.

28  Na ulimi wangu utanena haki yako, Na sifa zako mchana kutwa.


 SADAKA